Wednesday, May 15, 2013

WAANDAMANAJI NCHINI KENYA WAACHILIA NGURUWE KWENYE MAANDAMANO

Waandamanaji nchini Kenya waliwaachia nguruwe dazeni mbili kwenye milango ya bunge siku ya Jumanne (tarehe 14 Mei), wakamwaga damu kwenye sakafu wakilalamikia madai ya kupandishwa sana kwa mishahara ya wabunge wapya.
    Mwandamanaji mmoja akiwa ameinama karibu na nguruwe kwenye milango ya bunge tarehe 14 Mei wakati wa maandamano jijini Nairobi dhidi ya wabunge waliodai mishahara mikubwa. [Simon Maina/AFP]
  • Mwandamanaji mmoja akiwa ameinama karibu na nguruwe kwenye milango ya bunge tarehe 14 Mei wakati wa maandamano jijini Nairobi dhidi ya wabunge waliodai mishahara mikubwa.
"Hatutawaruhusu wabunge kujiongezea mishahara tukiwatazama tu," alipiga mayowe aliyepanga maandamano, Okiya Omtatah, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP. "Ni waroho kama walivyo hawa nguruwe tuliowaleta hapa."
Polisi waliwakamata watu 10, wakatumia gesi ya machozi kuwatawanya waandamaji na kuwapiga wengine kwa magongo. Kisha walikimbia nyuma ya nguruwe hao waliotanda kwenye eneo lenye majani linalozunguka jengo la bunge.
Mnamo mwezi Machi, Kamisheni ya Mishahara na Ujira (SRC) ilikata mshahara wa wabunge isiyokatwa kodi kutoka shilingi 851,000 (dola 10,100) kwa mwezi hadi shilingi 535,000 (dola 6,400).
Mithika Linturi, mbunge anayeunga mkono mswada wa kuifuta SRC, alisema waandamanaji hao walipaswa kutumia "njia muafaka kuwasilisha malalamiko yao."
"Kenya si taifa la ovyo ovyo. Eneo la bunge lazima liheshimiwe," alisema Linturi, akiongeza kwamba wabunge "wana haki ya kuwa na mawazo yao hata kama hayamfurahishi kila mtu."
Mswada huo ni wa kwanza kwa wabunge wa Kenya tangu uchaguzi mkuu wa tarehe 4 Machi.

No comments: