Ukiritimba na ukosefu wa ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam unaigharimu Tanzania na nchi jirani zaidi ya dola bilioni 2.6 (shilingi trilioni 4.3) kwa mwaka, kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa siku ya Jumanne (tarehe 21 Mei).Kuifanya bandari kuwa na ufanisi kama ule wa bandari ya karibu ya Mombasa kungeliweza kuokoa dola bilioni 1.8 (shilingi trilioni 2.9) za serikali, alisema mwanauchumi wa ngazi ya juu wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Jacques Morriset.
Bandari ya Dar es Salaam ni lango linalopitia asilimia 90 ya biashara ya Tanzania, ukipitisha mizigo yenye thamani ya dola bilioni 15 (shilingi trilioni 24.4) kwa mwaka, sawa na asilimia 60 ya pato jumla la Tanzania kwa mwaka 2012.
Licha ya hayo, ukosefu wa ufanisi unasababisha kuchelewa sana kwa bidhaa kuwafikia wateja, sio tu nchini Tanzania bali pia huko Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ukosefu wa ufanisi unaigharimu sana Afrika ya Mashariki, kwani wanalazimika kulipa zaidi kwa bidhaa zinazoingizwa, zikiwemo bidhaa za msingi kama mafuta ghafi, saruji, mbolea na madawa. Katikati ya mwaka 2012, meli zilikuwa zikingojea hadi siku 10 kwa uchache ili ziweze tu kutia nanga na siku nyengine 10 za ziada kupakua mizigo na kuondosha bidhaa zao, kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Waziri wa Usafirishaji, Harrison Mwakyembe, alisema yeye na mawaziri wengine sita watawajibika ikiwa hakutakuwa na uboreshaji kwenye bandari hiyo kufikia mwakani
. Alisema ufanisi kwenye bandari hiyo umeongezeka tangu kuondolewa kazini kwa maafisa wa bandari na kuteuliwa kwa bodi mpya ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari ya Tanzania mwaka huu, na aliapa kuzidisha maradufu kiwango cha bidhaa zinazopitia bandarini hapo.
Muda wa utoaji wa mizigo umeshuka kutoka siku 10 hadi 4.9 chini ya bodi hiyo mpya, alisema mjumbe wa TPA Jaffer Machano.
No comments:
Post a Comment