SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) limemteua ofisa wake mmoja aanze
kushughulikia suala la fedha zinazotokana na malipo ya mshambuliaji
Emmanuel Okwi wanazotakiwa kulipwa Simba.
Ofisa huyo anayejulikana
kwa jina la Mario Di Mangos ndiye atafanya kazi hiyo ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia inailipa Simba dola
300,000 (zaidi ya Sh milioni 480).
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amethibitisha kuhusiana na taarifa za Di Mango kupewa kazi hiyo na Fifa.
“Kweli, Di Mango ndiye atashughulikia suala hilo na Fifa wameahidi kuleta barua kuhusiana na uteuzi huo.
“Maana
Etoile Du Sahel wanataka kuleta mambo ambayo si sahihi, wanasema kuna
matatizo ya uhamishaji fedha sijui kuna masharti ya benki kuu
yanawabana. Sisi tunaona si sahihi na tunataka fedha zetu,” alisema
Rage.
Awali Simba ilikuwa imeteua wajumbe watatu kwa ajili ya kwenda Tunisia Mei 21 kwa ajili ya kufuatilia fedha hizo.
Etoile
du Sahel iliahidi kuilipa Simba kitita cha dola 150,000 kama awamu ya
kwanza na fedha hizo zilitarajiwa kutua nchini Januari 31 lakini mambo
hayakuwa hivyo kama ilivyokuwa kwa awamu ya pili ambayo wangelipa
Februari 28, mwaka huu.
Baada ya hapo, Simba imekuwa ikihaha kila
kukicha kupata fedha hizo na mara kadhaa imekuwa ikikumbana na ukata na
uongozi wa Rage umekuwa ukilalama kwamba unadai fedha nyingi kwa wadau
mbalimbali zikiwemo hizo za Okwi.
No comments:
Post a Comment