Wednesday, July 3, 2013

Nyerere, alikuwa hafungamani na upande wowote, sifa iliyoifanya Tanzania iheshimike, sasa hivi ni kama vile tumekosa muelekeo kabisa, hatujui tunaongozwa na itikadi gani. ni kama vile tunaongozwa na mkuu wa wilaya.

Inawezekana Serikali ikawa haishtushwi na mchezo wa triple K, kisa hasa ni kiburi cha kuwakumbatia mataifa makubwa mawili Duniani China na Marekani, na kuthibitisha hilo viongozi hao wamekuwa na mbwembwe sana kwa ziara zao zote walizofanya Africa, Wa Kiongozi wa China kufanya ziara yake ya kwanza nje kuwa Tanzania na Marekani kutumia muda mwingi tu ukilinganisha na nchi nyingine kufanya ziara Tanzania.


Kuna messages nyingi sana katika ziara za watu hawa. Bahati Mbaya sana ukiungana na Mataifa haya huwa huwajibiki kwa waliokkupigia kura bali unawajibika kwao, na hii ndio tofauti. Mambo mengi yanaweza yasiwe wazi kwa kigezo cha usalama wa nchi husika. Ingawa mchezo inaoucheza Tanzania na Mataifa haya makubwa mawili ni wa kutatansiha, lakini yawezekana kabisa ikanufaika. Hofu yangu ni kuwa bado kabisa hatujaweza kupenya vya kutosha kwenye masoko ya mataifa haya, na kwakuwa hatuzalishi kiviwanda kiasi cha kutosha na kuobora unaohitajika katika ushindani wa kimataifa, ni wazi tutategemea Kilimo kuexport. Hatari yake ni kuwa kilimo hicho sio kule cha bibi na babu yangu au mjomba wangu kule kijijini, ili tuweze kupata soko uwezekano mkubwa kwa kigezo cha ubora na kiwango watakuja wenyewe kulima na kuuza, na sisi tufaidike na kodi, ambayo kama hakutakuwa na Tax holiday basi itakuja mapema, jambo ambalo sina uhakika nalo.


Soko kubwa na la uhakika ambalo hata Mwalimu alilizungumzia na linaloweza kukuza uchumi kwa haraka ni soko la Afrika. Haya masoko hayajali sana ubora wa bidhaa zetu na hawawezi kuweka vikwazo vikubwa kiasi hicho labda kuwe na ushindani wa bidhaa za ndani na za nje ya nchi husika. Kenya iliwahi kufaidika sana na soko la Tanzania miaka ya 80 na 90, kwa kuingiza bidhaa za plastiki, sabuni na vipodozi ikiwa ni baadhi tu. Nadhani uhusiano wa triple K ni wa kuutizama kwa jicho a husuda na kuona ni jinsi gani tutamudu ushindani huu hasa biashara ya Bandari, na Reli ambayo tuliwahi kusikia Kagame na Museveni mara kadhaa wakijaribu kutushawishi tuijenge ili waitumie kwa bandari ya Tanga na Dar es Salaam. Wakati huo uhusiano wao na Kenya haukuwa mzuri sana. Kijana Uhuru naona anajua hili na sasa anatumia loophole ya ukiritimba wetu katika kukuza uchumi kutap opportunity ya kukuza biashara na chi hizi. Tusisahau tayari soko lao sasa linaenea Ethiopia na Sudani ya Kusini na hivi punde itakuwa Somalia, ni soko kubwa sana lenye walaji wengi tu ukilinganisha na majirani wetu wa kusini wa Zambia, Malawi na Msumbiji. Angalau Kongo tunaitegemea, na kama tutashinda vita kama walivyofanya Kenya.

Uhusiano wetu na Kenya na Rwanda umeingia doa kwa sababu kubwa mbili. Kwanza kuingia katika vita ya Kongo tayari kumemuudhi sana Kagame, ambaye ni rafiki ndugu wa Museveni kwa mengi tu. Uhusiano wetu na mataifa ya Magharibi unatudhibiti sisi kuikumbatia Kenya ambayo kiongozi wake ni mshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa. Watatu hawa wanalijua hili na kauli ya JK ilitia msumari wa moto kwenye kidonda kibichi cha Kagame na Uhuru.

Ni pale ambapo tutapata Kiongozi mpya baada ya uchaguzi na ambaye ana siasa zisizofungamana na upande wowote na ambaye anajali uchumi zaidi kuliko Siasa, ndipo tutashuhudia mabadiliko. Kwa sasa kiongozi wetu anasimamia Siasa zaidi katika kukuza uchumi na hilo anaonekana kufanikiwa ingawa wachunguzi wa mambo tayari wanamkosoa kwa kukumbatia siasa na matabaka kimyakimya bila kuwa muwazi kama kiongozi katika kutoa muelekeo wa mambo ya Kitaifa. Anachukuliwa kuwa mtu mwenye kupuuzia mambo mengi nyeti yanayoathiri Siasa na Uchumi wa nchi mpaka pae yanapokuwa ya moto, mtu ambaye yawezekana akawa hapendi kulaumiwa kwa jambo lolote.

Wasiwasi mkubwa na kuwa kila wanapofika viongozi wa mataifa haya makubwa Duniani wanasaini Mikataba kedekede, ambayo wananchi wengi hawajashiriki na aghalabu inajulikana undani wake. Je ujio huu na kusainiwa kwa mikataba hii hakutaathiri muelekeo wa kiuchumi na kisisasa wa miaka ijayo hata kama JK akiwa hayupo madarakani? Je ni mipango yenye nia njema ya muda mrefu au ni kama ile ya kupofusha macho na tuanpokuja kujua tunakuwa tumechelewa? Hatujui, maswali haya yatajibiwa tu na kauli za JK katika hotuba zijazo na kutueleza kinagaubaga nini anachokifanya sasa kwa lugha nyepesi huku akitambua kuwa anawajibika kwetu na si kwa wangine.


;source profesa.

No comments: